FLASH


Sunday, February 3, 2013

SAKATA LA MITAALA NA UBORA WA ELIMU



Lowassa amuunga mkono Mbatia 

NI KUHUSU UBOVU WA MFUMO WA ELIMU,ASEMA WABUNGE WENGI WANATAKA MITAALA IANGALIWE UPYA

Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, akimkabidhi cheti mwanafunzi bora, Danny Kitalika wakati wa mahafali ya 13 ya Kidato cha Sita Shule ya Sekondari ya Benjamin William Mkapa yaliyofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi wa Shule hiyo, Maneno Mbegu. Picha na Venance Nestory 
Na Ibrahim Yamola  (email the author)


WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameunga mkono hoja binafsi ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia kuhusu udhaifu wa elimu nchini akisema, kuna udhaifu mkubwa katika sekta hiyo.
Lowassa alisema hayo jana katika Mahafali ya 13 ya Kidato cha Sita ya Shule ya Sekondari Benjamini William Mkapa, jijini Dar es Salaam ambapo alieleza kuwa sekta ya elimu inahitaji kufanyiwa marekebisho ili kuweza kuzalisha wahitimu wenye tija kwa taifa.
”Kuna tatizo la hali ya elimu nchini, tushirikiane wazazi, jamii, wanasiasa na wataalamu, tuangalie jinsi ya kusaidia sekta ya elimu kwa maana tutasaidia watoto wa nchi yetu,”alisema Lowassa.
Katika mahafali hayo, Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli mkoani Arusha kupitia (CCM) aliwakabidhi vyeti jumla ya wahitimu 330, kati yao wavulana 263 na wasichana 67 .
“Wabunge wengi bungeni tunakubaliana kwamba ipo haja ya kutazama upya suala zima la mitalaa ya elimu katika nchi yetu kwani elimu iliyopo inawaandaa watafuta kazi na siyo wanaotaka kujiajiri,”alisema Lowassa.
Alisema kuwa kukiwa na mfumo mzuri wa elimu wenye kuwaandaa wahitimu walio na uwezo wa kujiajiri wenyewe na kutokutegemea kuajiriwa taifa litapiga hatua.
Alihamisi wiki hii, Mbatia aliwasilisha bungeni Hoja Binafsi kuhusu Udhaifu wa Elimu Tanzania, akitaka mfumo mzima unaosimamia elimu nchini ufumuliwe, hoja iliyogeuka ‘kaa la moto’ kwa Serikali.
Baada ya majadiliano marefu kuhusu kuundwa kwa kamati ya kuchunguza mitalaa, sera na mihutasari ya elimu, hoja mbalimbali zilitolewa, huku baadhi ya wabunge wakitaka Kamati ya Bunge, wengine wakitaka iundwe tume huru ya kufuatilia suala hilo.
Mjadala huo uliendelea juzi asubuhi kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kusimama na kutetea mfumo wa elimu uliopo na kusisitiza kuwa Serikali inayo mitalaa, kabla ya wabunge kuchangia na Mbatia kuhitimisha akitaka kuiondoa hoja yake hadi Serikali itakapowasilisha mitalaa hiyo ya elimu bungeni.
Hata hivyo, Naibu Spika, Job Ndugai alikataa pendekezo la Mbatia na kutumia kanuni za Bunge za kuipitisha hoja hiyo kwa kuwahoji wabunge.
Baada ya hoja hiyo kupitishwa kwa kuungwa mkono na wabunge wengi wa CCM, hali hiyo iliwaudhi wabunge wa upinzani, ambao waliamua kutoka nje ya ukumbi.
Baadaye walikubaliana kumshtaki Waziri Kawambwa kwenye Kamati ya Bunge ya Mamlaka ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, wakimtaka ajiuzulu kwa kulidanganya Bunge, ikishindikana watalipeleka suala hilo kwa mamlaka zilizomteua. 
(chanzo gazeti la mwananchi)

No comments:

Post a Comment