FLASH


Sunday, January 20, 2013

KWA MWENDO HUU TUTAENDELEA KUSHINDA TU

MJUMBE WA MKUTANO MKUU CHADEMA AACHIA NGAZI CHEO NA UANACHAMA

*Awaponda Sugu na Msigwa kwa kutotekeleza ahadi zao kwa wananchi MBEYA, Tanzania
                                                                      Edo Mwamalala
 MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chadema, Taifa, Edo Mwamalala, ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo, huku akimtaka Mbunge wa jimbo la Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu', kufanya kazi ya kutekeleza ahadi zake na za CHADEMA, alizotoa kwa wananchi badala ya kuwajengea mfumo wa kufanya fujo.

Sambamba na Sugu mbunge mwingine aliyetakiwa kufanya hivyo ni mchungaji Peter Msigwa wa jimbo la Iringa mjini kupitia CHADEMA.

Akitangaza, kujiuzulu kwake mbele ya waandishi wa habari, Mwamalala pamoja na ujumbe wa Mkutano pia amejivua uanachama wa Chadema.

Mwamalala alisema wabunge hao wawili, waliwaahidi wananchi wa majimbo ya Mbeya mjini na Iringa mjini ahadi kadhaa, wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, lakini hadi leo hakuna lolote la maana walilolifanya.

Alisema Mbilinyi aliwaahidi wananchi wa jimbo la Mbeya mjini, kuhusu kujenga bandari kavu, masuala ya elimu, Maji safi na salama, afya, amani, upendo na kukuza vipaji vya wasanii Mbeya mjini, lakini hadi leo hakuna lolote aliloweza kulitekeleza.

“Mbilinyi na mchungaji Msigwa wanatakiwa wafanye kazi ya kutekeleza ahadi zao na CHADEMA, lakini siyo leo hii waanze kuwajengea wananchi mfumo wa fujo” alisema Mwamalala.

Aliongeza uongozi wa wilaya ya Mbeya mjini ni wa mapinduzi kila kukicha na hivyo kuufanisha sawa na utawala wa Wasomalia, huku akiwaponda viongozi waliopo kuwa ni makanjanja wa kupindua wenzao kwa uroho wa madaraka.

Aliongeza ujanja wa viongozi wa CHADEMA kuwateka wananchi na shida zao kupitia majukwaa ya siasa unatakiwa uwe na huruma, hivyo wakae chini na kuanza kuendesha siasa za maendeleo na siyo kuwaza fujo na matusi.

Alisema ni vyema viongozi na wana-CHADEMA wajifunze kutenganisha maendeleo yanayoletwa na serikali kuu kama ujenzi wa barabara za jiji la Mbeya kwa kiwango cha lami na ubunge kama taasisi.

Alimtuhumu Sugu kuwa amekuwa na tabia ya kuwahadaa wananchi kuwa barabara kadhaa zinazojengwa mjini Mbeya kwa kiwango cha lami, ni juhudi zake wakati mchakato wa kuzijenga chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia (WB), ulianza tangu mwaka 2008 wakati huo hana hata ndoto ya kuja kuwa mbunge.