FLASH


Saturday, February 16, 2013

WASEMAVYO BAADHI YA WAHARIRI

VIGOGO WAPYA WA KUWANIA URAIS NDANI YA CCM

Kwa ufupi

NI DK SALIM,NCHIMBI,MWINYI,MIGIRO NA WASSIRA.
 

UCHAGUZI wa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) uliofanywa na Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho Jumatatu wiki hii mjini Dodoma, ni kama unabadili mwelekeo wa siasa za ndani za chama hicho kikongwe nchini.

Tangu Rais Jakaya Kikwete aingie madarakani miaka saba iliyopita na kupewa kofia ya uenyekiti wa CCM, chama hicho kimekuwa kwenye minyukano ya siasa za visasi kiasi kwamba hakijawahi kuwa na utulivu wa kisiasa kama ilivyo sasa, miezi michache baada ya kufanyika mabadiliko kadhaa ya kiuongozi.

Uteuzi na baadaye uchaguzi wa wajumbe wa Kamati Kuu umeweka kando baadhi ya vigogo wa kisiasa hasa waliokuwa wakitajwa katika harakati za kuusaka urais katika uchaguzi wa 2015 na kuziingiza sura mpya ambazo huenda baadhi yao wanaweza kuingia katika kinyang’anyiro hicho.

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ni vigogo ambao wamekuwa wakitajwa kupiga mbio hizo, lakini waliwekwa kando katika     Kamati Kuu ya sasa.

Pia majina ya mawaziri na wizara zao kwenye mabano Profesa Mark Mwandosya (Ofisi ya Rais – Kazi Maalumu), Dk John Magufuli (Ujenzi), Dk Harrison Mwakyembe (Uchukuzi) pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela, pia hayakuwa sehemu ya waliopendekezwa kuingia katika CC ambacho ni chombo cha kufanya uamuzi mkubwa ndani ya CCM.

Profesa Mwandosya licha ya kuwa na matatizo ya kiafya, amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa watu muhimu katika mustakabali wa siasa za sasa za Tanzania wakati Dk Magufuli na Dk Mwakyembe wamekuwa wakipigiwa chapuo na umma kwamba huenda wangefaa kuwania urais kutokana na kasi katika utendaji kwenye wizara wanazoziongoza.

Badala yake Kamati Kuu inawajumuisha makada ambao siyo wapya, lakini ambao wanaweza kutumika kubadili sura na mwelekeo wa siasa ndani ya CCM hasa tunapoelekea 2015, akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Dk Salim Ahmed Salim.

Hatua hiyo inaweza kuwa ni hatua ya kujaribu kujipanga kwa CCM katika kuzipa sura mpya siasa za ndani ya chama hicho. Dk Salim kama ilivyo kwa Profesa Mwandosya, alikuwa mpinzani wa Kikwete katika kinyang’anyiro cha urais wa 2005, ambaye bado anatizamwa kuwa mtu mwenye uwezo licha ya kwamba umri wake ni mkubwa.

Wengine ambao kuingia kwao katika Kamati Kuu ya CCM kunaweza kuwa na maana ya kubadili siasa za urais ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi na mwenzake kutoka Tanzania Visiwani ambaye alipata kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha.

Dk Nchimbi anarejea Kamati Kuu ambako aliingia kwa mara ya kwanza akiwa na umri mdogo pale alipochaguliwa kuongoza Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na kuongoza jumuiya hiyo kwa miaka kumi mfululizo. 

Kwa mujibu wa kanuni za CCM, wenyeviti wa jumuiya za chama huwa ni wajumbe wa CC kwa mujibu wa nyadhifa zao.  Nchimbi amekuwa mjumbe wa CC kwa miaka 10.

Hali kadhalika, Dk Mwinyi ni mmoja wa makada wa CCM ambaye amekuwa ndani ya CC kwa muda mrefu, wakati Nahodha alikuwa akiingia ndani ya kamati hiyo alipokuwa Waziri Kiongozi wa SMZ (kwa wadhifa wake).

Nahodha, Dk Mwinyi na Dk Nchimbi kwa nyakati tofauti wote wamepita katika wizara nyeti ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Dk Mwinyi wakati alipokuwa waziri, naibu wake alikuwa Dk Nchimbi ambaye baadaye alihamishiwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na sasa Mambo ya Ndani.

KWETU PAZURI

KARIBU CCM JULIANA SHONZA NA  

MTELA MWAMPAMBA    

Juliana Shonza akijitambulisha kwa wana CCM  tarehe 12/2/2013, katika Makao Makuu ya CCM,mjini Dodoma
Mtela Mwampamba akijitambulisha kwa wana CCM,wakati wa sherehe za utambulisho wa  wajumbe wa kamati kuu ya CCM.

Mwenyekiti wa CCM-Taifa,Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa kwenye picha ya pamoja na wanachama wapya  wa CCM,Juliana Shonza na Mtela Mwampamba,kushoto kwenye picha ni Makamu Mwenyekiti CCM-Bara ,Ndugu Philip Mangula na kulia ni Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Abdulrahaman Kinana.
Mwenyekiti wa CCM-Taifa,Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wananchi wa Dodoma wakati wa sherehe za kuipongeza Kamati Kuu iliyochaguliwa jana mjini Dodoma.

TAMKO LA CCM

TAMKO LA HALMASHAURI KUU YA CCM TAIFA KUHUSU MAANDAMANO NA VURUGU ZILIZOTOKEA MKOANI MTWARA JUU YA UJENZI WA BOMBA LA GESI NA MAENDELEO YA MTWARA    

Katibu wa NEC,Itikadi na Uenezi,Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Sekretarieti ,Makao Makuu ya CCM ,Dodoma leo tarehe 13/2/2013. 

TAMKO LA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CCM KUHUSU MAANDAMANO NA VURUGU ZILIZOTOKEA MKOANI MTWARA JUU YA UJENZI WA BOMBA LA GESI
NA MAENDELEO YA MKOA WA MTWARA
1.       Halmashauri Kuu ya Taifa imepokea maelezo ya Serikali kuhusu maandamano na vurugu zilizotokea Mkoani Mtwara tarehe 27 Desemba, 2012 tarehe 25 Januari, 2013 na tarehe 26 Januari, 2013. Maandamano na vurugu hizo zilizodaiwa kuwa na lengo la kupinga mradi wa bomba la Gesi kujengwa na kupeleka Gesi Dar es Salaam.
2.       Baada ya kupokea maelezo haya ya Serikali, Halmashauri Kuu ya Taifa imebaini kuwa: -
(a)           Kwa sehemu kubwa Wananchi wa Mkoa wa Mtwara hawakuwa wamepewa elimu ya kutosha juu ya uendelezaji wa Gesi na jinsi watakavyonufaika.
(b)           Baadhi ya Wanasiasa na baadhi ya Viongozi wa Makundi mbalimbali waliamua kutomia suala la Gesi kupandikiza lugha za chuki, uchochezi na upotoshaji wa maendeleo ya Mradi wa Gesi kwa lengo la kujitafutia umaarufu.
(c)            Suala la Gesi limetumika kama kisingizio tu cha kufanya vitendo vya rurugu na uvunjifu wa amani.
3.       Kutokana na ukweli huu, Halmashauri Kuu ya Taifa inaelekeza ifuatavyo:-
(i)             Imesikitishwa na vurugu zilizotokea na kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha na uharibifu mkubwa wa mali  na majengo  ya CCM, Serikali, Wabunge na watu binafsi. Halmashauri Kuu ya Taifa inawapa pole wafiwa na waliopoteza mali zao.
(ii)      Inaiagiza Serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu waliofanya vurugu na uharibifu mbalimbali na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa Sheria. Pia, kuwa makini na kuhakikisha matukio kama haya hayajitokezi tena.
(iii)        Inaiagiza Serikali kuendelea kutoa elimu ya kutosha kwa Wananchi wa maeneo husika  kuhusishwa na kuelimishwa juu ya miradi mbalimbali kwenye maeneo yao.
(iv)        Halmashauri Kuu ya Taifa inawataka Wananchi wa Mkoa wa Mtwara kuendelea kuishi kwa amani na utulivu kama ilivyo desturi yao, maana vurugu pamoja na kuharibu mali na kugharimu maisha  vinaweza kuwakimbiza wawekezaji waliojitokeza na ambao  shughuli zao zitawafaidisha  wananchi wa Mkoa huu na Watanzania kwa ujumla .
HALMASHAURI KUU YA TAIFA
Dodoma 10 – 11 Februari,2013