UVCCM IRINGA NA MBEYA WAKATAA ZIARA YA VIONGOZI WAO WA KITAIFA
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Hamis Sadifa.
KATIKA mwendelezo wa mnyukano wa hisia
za viongozi wa Umoja wa vijana Taifa (UVCCM) kushinda uchaguzi kwa
rushwa, baadhi ya viongozi wa umoja huo katika mikoa ya Iringa na Mbeya
wameikataa ziara iliyotarajia kufanyika katika mikoa hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi
ya wajumbe wa mabaraza ya mikoa na mkutano mkuu wa taifa, walisema kuwa
ziara hiyo haina maana yeoyote kutokana na viongozi hao kuwa watuhumiwa
wa rushwa.
Baadhi ya wajumbe kutoka mkoa wa Iringa
wakiwemo baadhi ya makatibu wa wilaya walisema kuwa Mwenyekiti wa UVCCM
Taifa Hamis Sadifa na wenzake ni mmoja kati ya viongozi waliokuwa
wanataka kulinda na kutetea ufujaji wa mali za umoja huo mkoani Iringa
hasa mradi wa mashamba ambayo mmoja wa viongozi wa umoja huo alikuwa
akiutumia kama mali yake binafsi hali ambayo ilipelekea Mwenyekiti wa
UVCCM mkoa wa Iringa Tumaini Msowoya kusimama kidete na kuhoji hali
ambayo akaonekana hafai kwasababu hakutakiwa kuhoji.
Baadhi ya makatibu wa wilaya hiyo
walisema kuwa kipindi hiki ni cha kilimo hivyo ziara hiyo haina maslahi
kwa vijana wa chama hicho kinachohamasisha vijana kufanyakazi badala ya
maandamano na kuzurula kwenye misafara.
Katika mkoa wa Mbeya baadhi ya wajumbe
wa baraza la vijana walisema kuwa ziara hiyo hawaitaki kwasababu
mbalimbali ikiwemo sababu waliyodai kuwa ni kubwa waliyoitaja kuwa ni
ziara hiyo kufedhehesha chama kwa kuwachangisha wadau fedha kwa ajili ya
malazi, safari na hata chakula.
walisema kuwa wanatambua kuwa viongozi
hao wa kitaifa wanapofanya ziara huwa wanakuwa na mafungu yao lakini
wameshangazwa kupata barua na maelekezo kutoka ofisi za mkoa kuwa jukumu
la kuwalaza, kuwalisha na kuwasafirisha vigogo hao inabidi zigharamie
wilaya kinyume na taratibu huku viongozi wa mkoa wakizidi kuomba
michango mpaka huko wilayani ambapo katika wilaya ya Ileje kuna barua
iliyokuwa ikielekea kwa Mkuu wa wilaya hiyo ilichanwa.
Baadhi ya wajumbe kutoka wilaya ya Mbeya
vijijini walisema kuwa hawapo tayari kuwapokea viongozi hao wa kitaifa
kutokana na sababu hiyo na pia mgeni aliyepangiwa kutembelea wilaya hiyo
alikuwa ni Makamu Mwenyekiti Taifa Mboni Mwita ambaye tangu uchaguzi
mkuu ulipofanyika mjini Dodoma, mkoa wa Mbeya uliongoza kumkataa hata
kufikia hatua ya kutaka kupigana na wapambe wake wa baadhi ya mikoa kwa
madai kuwa uchaguzi huo ulitawaliwa na rushwa katika nafasi yake hali
ilyonusuriwa na usalama wa taifa na msimamizi wa uchaguzi huo William
Lukuvi.
Ziara hiyo kwa mkoa wa Mbeya imeelezwa
kuwa ingetakiwa kufanyika tangu tarehe 3-4-2013 lakini ikaahirishwa na
kupangwa tarehe 13-4-2013 lakini pia imeahirishwa kutokana na kile
kilichodokezwa kuwa ni kutokana na baadhi ya vigogo wa umoja huo taifa
kuhojiwa na kamati ya maadili.
Hata hivyo ziara hiyo endapo kama
itafanyika mkoni Mbeya inaelezwa kuwa itatawaliwa na malumbano kutokana
na jinsi ilivyopangwa na kuwakwepesha baadhi ya viongozi wakuu na
kuwapeleka katika wilaya za pembezoni ambako vijana wengi hawaweze
kuwahoji vema viongozi hao.
Kwa mfano mwenyekiti wa Taifa alipangiwa
wilayani Kyela na Mbarali na kumkwepesha Mbeya Mjini ambako inaonekana
kuwa Mwenyekiti huyo hana mahusiano mema na Mwenyekiti wa wilaya hiyo
aliyetajwa kwa jina la Matukuta huku katibu Mkuu Martin Shigela naye
akikimbiziwa Ileje, Momba na Mbozi.
Mbali na viongozi hao kukimbiziwa katika
wilaya za nje ya mji, pia hawapo katika ziara ya kuzungumza na wasomi
wa vyuo na vyuo vikuu.
Mpaka sasa michngo ya kugharamia ziara
hiyo ''mfu'' inaendelea kuchangishwa huku wahusika wakiwa ni makatibu na
wenyeviti wa jumuiya hiyo.
Wakati huo huo, taarifa zilizokifikia
kikosi kazi cha mtandao wa www.kalulunga.com zimeeleza kuwa katibu wa
wilaya ya Mbarali aliyetajwa kwa jina la Mwajuma amejiuzulu na kuacha
kazi ya umoja huo kwa madai kuwa anataka kushughulika zaidi na familia
yake.